Na Mwandishi wetu
MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam,Albert Chalamila amemtaka mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kimara Bonyokwa na Kinyerezi kuhakikisha anamaliza ujenzi huo kwa wakati na viwango vya juu kama mkataba unavyomtaka.
Pia mradi huo wenye thamani ya bilion 24.03 kujenga barabara zenye urefu kilomita 8 daraja moja la Kinyerezi, makalavati saba na taa za barabarani.
Akizungumza leo March 9,2024 jijini Dar es Salaam Chalamila wakati wa Hafla ya kumkabidhi mkandarasi mradi wa barabara hiyo amesema barabara hiyo ilikuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wakazi wa kimara.
“Hii barabara imekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wakazi wa eneo hili tulikuja hapa kipindi mvua zilivyonyeesha wananchi wakatununia lakini ilikuwa ni wajibu wao kufanya hivyo sasa wakati wakufurahi umefika,”amesema Chalamila.
Amesema mkandarasi anapaswa kufanyakazi usiku na mchana ili kuhakikisha barabara hiyo inakamilika ndani ya miezi 16 na kuahikisha pindi mvua zitakaponyeesha ikute barabara imeanza na inakaribia kukamilika ili wananchi wasipate usumbufu.
Aidha Chalamila amesema amepata taarifa kuwa kunabaadhi ya wakazi wa eneo hilo wameishtaki Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD) hivyo amesema wataendelea kusikiliza maamuzi ya mahakama na pindi hukumu ikitoka kama TANROAD imeshinda basi atachukua hatua za haraka kuhakikisha anaboma nyumba zote kwenye eneo hilo.
“Nimepata taarifa kuwa kuna baadhi ya wakazi wa hapa wameenda kuishtaki TANROAD jambo zuri sana ila niwahakikishie endapo hukumu itatoka TANROAD imeshinda sitachukua hata dakika 10 nitakuwa nimeshafika hapa na kijiko sitaangalia nini kimetoka au nani yupo ndani nitavunja zote ,”amesema.
Sambamba na hayo Chalamila amewataka wananchi kuchagua viongozi ambao wataendelea kuwaletea maendeleo na si kuwagawa na kuwacheleweshea maendeleo.
Pia ametoa Rai kwa viongozi wa vyama vya siasa hasa CCM kuacha figusi wanazozifanya ndani ya chama na kusababisha kuchelewesha maendeleo kwa wananchi na pia vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama.
Naye Mbunge wa Jimbo la Segerea Bona Kamoli amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha pesa kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara hiyo huku akitoa wito kwa serikali kuhakikisha wanakarabati mto Msimbazi kwani umekuwa ukiwafuata wananchi na si wananchi kufuata mto kama ilivyokuwa awali.
Amesema barabara ikikamilika itaongeza uchumu kwa wakazi wa maeneo hayo kwani watakuwa na uwezo wa kufanyakazi muda wote lakini hata watu wataongezeka kwani watakuwa na uhakika wa usafiri.
Ameongeza kuwa mchakato utakaoanza wa mradi wa DMDP unatarajiwa kuanza mwezi wa nne hivyo wanaomba mchakato huo usipelekwe mbele huku wakiomba Mungu mvua zisinyeenye kwa kipindi hiko ili barabara za mitaa zikamilike.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ubungo Profesa Kitila Mkumbo amesema ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwani hiyo ilikuwa moja ya ahadi ya chama kwa wananchi wake.
“Ujenzi wa barabara hiI unaanza rasmi leo Machi 9 mwaka huu hawatarajii kusimamishwa hadi utakapokamilika na kukabidhiwa lakini pia kuhakikisha wanatoa ajira kwa vijana wa jimbo la ubungo na Segerea,” amesema Profesa Mkumbo.
Akizungumzia ujenzi wa barabara hiyo Mkurugenzi wa Barabara TANROAD Mhandisi Jephason Nnko amesema ujenzi wa barabara hiyo utahusisha na ujenzi wa daraja la Kinyerezi, makalavati, barabara ya watembea kwa miguu na kuwekwa kwa taa barabara yote ili kusaidia hata wafanyabiashara kuweza kufanyabiashara zao wakati wote.
Kwa upande wake Meneja Mradi waKampuni ya Ujenzi Nyanza, Mhandisi Gilbert Bahesha amesema watahakikisha historia inaendelea kuandikwa katika barabara hiyo kwani wanatarajia kumaliza mradi huo kwa wakati uliopangwa ili kuendelea kukata kiu ya wananchi hao.