Home KITAIFA WANAWAKE TARURA WATEMBELEA GEREZA LA WANAWAKE ISANGA

WANAWAKE TARURA WATEMBELEA GEREZA LA WANAWAKE ISANGA

Na Mwandishi wetu, Dodoma

WATUMISHI wanawake wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wamepongezwa kwa kuwawezesha wanawake wenzao waliopo kwenye gereza la wanawake la Isanga jijini Dodoma.

Wanawake wa TARURA wametembelea gereza la wanawake Isanga leo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika Machi 8, kila mwaka

Kamishna Msaidizi wa Magereza na Mkuu wa Gereza Kuu-lsanga, Dodoma ACP. Zephania Neligwa amewapongeza wakati alipokea mahitaji mbalimbali kutoka kwa watumishi wanawake wa TARURA Jijini Dodoma.

ACP. Neligwa amesema mahitaji hayo yataenda kuwasaidia wanafunzi wao ambao ni wafungwa na mahabusi waliopo mafunzoni katika gereza la wanawake na kuongeza kwamba mahitaji hayo yatatumika ipasavyo.

“Mnapokuwa mnaadhimisha siku ya wanawake duniani sisi magereza tunaendeleza programu za urekebu kwa kuwajengea uwezo na ujuzi mbalimbali wanawake hawa ili hata watakaporudi uraiani waendelee kuzalisha na kuwa wajasiliamali,”amesema.

Naye, Afisa Utumishi wa TARURA, Ntuli Mwasalyanda amesema wao kama watumishi wanawake wanapoelekea kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani wameona ni vyema kuwagusa/kuwafikia wanawake wenzao waliopo gereza la wanawake –Isanga.

“Tumeona ni jambo jema kuadhimisha siku ya wanawake duniani na wanawake hawa ili wajione kwamba nao ni sehemu ya wanawake waliopo uraiani, watambue kuwa jamii haijawatenga na ipo nao, tumefurahi kwa kuona wanajishughulisha na shughuli mbalimbali,”amesema.

“Tumefurahi namna wanawake hawa walivyowezeshwa kwa kufanya stadi mbalimbali za mikono ambazo zinawaletea maendeleo ikiwemo ujuzi baada ya kutoka magereza,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mratibu wa Magereza na Mkuu wa sehemu ya wanawake SO. Sifa Anyimike amewashukuru watumishi hao wanawake wa TARURA.

“Kwa kuwatembelea wanafunzi waliokinzana na Sheria katika gereza hili,” amesema.

Amebainisha lengo la mafunzo wanayoyapata wanawake hao ni kuwasaidia watakaporudi uraiani kwa kuwawezesha kujiunga na vikundi vingine vya wanawake wajasiliamali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here