Home KITAIFA Nchimbi Marekani ni rafiki zetu

Nchimbi Marekani ni rafiki zetu

Na Mwandishi wetu,

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema dhamira ya Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nchi inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na utawala bora na hivyo haipaswi kutiliwa shaka hata kidogo.

Hayo ameyasema jana Machi 5 2024 kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba jijiniDar es Salaam na Katibu Mkuu huyo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle,ambapo viongozi hao walijadiliana masuala anuai kuhusu ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

“Katika utekelezaji wa dhana ya utawala bora, chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia, Tanzania imeendelea kushuhudia kuwapo kwa uhuru wa mihimili mitatu ya dola, ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama,” amesema Balozi Dk.Nchimbi.

Amesema mihimili hiyo ya dola imeendelea kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi vizuri na hivyo kuaminiwa na wananchi.

Balozi Nchimbi amesisitiza kuwa CCM chini ya Rais Dk.Samia, kitahakikisha dhamira hiyo pia inaendelezwa kwa vitendo kwa kuunga mkono uwapo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kwa maslahi ya nchi na taifa kwani umoja huo ni zaidi ya vyama vya siasa.

Katika mazungumzo yao, wamekubaliana nchi zote mbili kuangalia maeneo yanayoweza kuboreshwa kwa manufaa ya pande zote mbili hasa katika nyanja za biashara, uchumi na uwekezaji.

Vilevile, viongozi hao kwa pamoja wameelezea umuhimu wa kurahisishwa kwa upatikanaji viza.

“Ni wajibu wetu kuimarisha na kuuboresha uhusiano huu wa muda mrefu kama tulivyoupokea kutoka kwa waasisi na watangulizi wetu kama ulivyosema balozi. Tuuboreshe kwa ajili ya manufaa ya wananchi wetu wa pande zote mbili,” amsema .

Kwa upande wake Balozi Battle aliupongeza uongozi wa Rais Dk.Samia kwa jinsi ambavyo umekuwa wa wazi, imara na jasiri katika kusimamia misingi ya demokrasia na utawala bora.

“Kama unavyojua uhusiano huu ni wa muda mrefu, ukaboreshwa zaidi na urafiki uliokuwapo kati ya Mwalimu Nyerere na John Kennedy. Lakini pia kulikuwa na ukaribu kati ya Jakaya Kikwete na George Bush na sasa tunaona ukaribu kati ya Rais Dk. Samia na Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris. Napenda kukuhakikishia na ujue kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Marekani ni mkubwa na halisi,” amesema Balozi Battle.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here