Home KIMATAIFA Viwango vya kubadilisha fedha vyakuza deni nchi za Afrika

Viwango vya kubadilisha fedha vyakuza deni nchi za Afrika

Na Mwandishi wetu, Zimbabwe 

MADENI ya nchi nyingi za Afrika yanakua kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa viwango vya riba na kubadilisha fedha duniani na kusababisha kushuka kwa thamani ya fedha za ndani.

 Hayo yamebainishwa Mjini Victoria Falls, Zimbabwe, na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,  Elijah Mwandumbya, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu  Nchemba, wakati wa Mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi kutoka nchi za Umoja wa Afrika unaoratibiwa na Kamisheni ya Uchumi chini ya Umoja wa Mataifa (UNECA)

Mwandumbya amesema kuwa awali ukuaji wa deni ulikuwa unaendana na ukopaji lakini kwa sasa imebainika kuwa kuna sababu zingine zinazochochea kuongezeka kwa deni hilo ikiwa ni pamoja na mabadiliko makubwa ya viwango vya kubadilisha fedha na riba hivyo kuzifanya nchi za Afrika kutafuta njia mbadala ya kutatua changamoto hiyo.

Amesema kuwa katika kulihudumia deni “dept service” lililoongezeka, kumekuwa na changamoto kubwa kwa sababu nchi nyingi bado hazina uwezo wa kukusanya mapato ya kutosha kuweza kugharamia huduma mbalimbali.

“Sisi Tanzania tunashukuru kwa kuwa kupitia Taasisi za Kimataifa za Moody’s na Fitch zinazojihusisha na ufanyaji tathimini kwa nchi ili kujua uwezo wake wa kukopesheka katika masoko ya fedha ya Kimataifa, wamethibitisha kwamba nchi yetu ipo kwenye viwango vizuri vya kuweza kuendelea kukopesheshwa miongoni mwa nchi chache,”amesema Mwandumbya.

 Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuelekeza vyema kwenye suala hilo na hatimae nchi kuweza kuwa na viwango vya deni ambavyo ni himilivu na vinavyokubalika kimataifa.

 Mwandumbya amesema kuwa katika kukabiliana na changamoto za ukuaji wa madeni hususani kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya tabianchi ni lazima nchi za Afrika kuwa na mkakati wa kuhakikisha zinapata rasilimali fedha ili mipango inayotekelezwa iweze kukidhi mategemeo ya wananchi.

“Changamoto kubwa ambayo tunaiona hapa kwa nchi zetu za Afrika ni ile haja ya kuendelea kukusanya mapato ya kutosha ili kujihakikishia kwamba tunaweza kupata rasilimali za kuweza kuhudumia deni lakini pia tunaweza kulipa mishahara pia kuhudumia gharama mbalimbali za kibajeti,”ameongeza. 

 Amesema katika mkutano huo agenda kubwa inayojadiliwa ni kujaribu kupata suluhu ya namna gani nchi zitaboresha viwango vya ukusanyaji wa mapato ili kutoka kwenye viwango vya chini ya asilimia 11 na 12 ya Ukuaji wa Mapato ya Ndani (GDP) kwenda viwango ambavyo vinavyokubalika kuanzia asilimia 16.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk. Tausi Kida amesema kuwa dhumuni la mkutano huo wa 56 ni kubadilishana mawazo na hasa kwenye kauli mbiu inayosema Financing the Transition to Inclusive Green Economies in Afrika inayotoa hamasa na kutafakari njia ambazo zinaweza kutumika kufadhili Uchumi na kufanya uwekezaji ambao unazingatia mabadiliko ya tabianchi.

“Tunaendesha Uchumi kwa njia ya kodi kwa hiyo tunapambanua ni jinsi gani tutaweza kuboresha masuala ya utawala wa kodi katika nchi za Afrika kuweza kuongeza wigo wa kodi lakini vilevile kuhakikisha kodi inayokusanywa inaenda kwenye malengo kusudiwa, “ameeleza Dk. Kida.

 Aidha amesema kuwa kwenye mkutano huo wameweza kuona njia nyingi mpya zinazoibuka za kusaidia uchumi hususani mikopo nafuu kwenye uchumi wa kijani ambayo inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kufadhili mipango na miradi ya maendeleo.

Mkutano huo wa 56 unaoratibiwa na UNECA ni Jukwaa ambalo limeanzishwa na Umoja wa Mataifa ili kuzisaidia nchi za Afrika kufanya mijadala na tafiti mbalimbali ili kuzalisha na kufanya ubunifu utakaokuza uchumi hivyo kutengeneza fursa ya kujadiliana na kuhakikisha ushauri unaotolewa unaendana na mazingira halisi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here