Home KITAIFA Matokeo ya Royal Tour ya dhihirika Kilwa,Wimbi la watalii wa nje...

Matokeo ya Royal Tour ya dhihirika Kilwa,Wimbi la watalii wa nje lazidi kuonezeka

Na Beatus Maganja, Kilwa

KAZI ya kutangaza Utalii wa Nchi yetu iliyofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Tanzania “The Royal Tour” inazidi kudhihirisha matokeo chanya katika Hifadhi zetu Nchini hususan Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara ambayo inazidi kupata idadi kubwa ya watalii kutoka Mataifa mbalimbali Duniani Kila uchwao.

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA ) Februari 24, 2024 imepokea Kundi la sita la watalii wa kigeni wapatao 146 waliotoka ughaibuni kwa ajili ya kutembelea na kutalii ndani ya Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara iliyopo wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.

Imetajwa kuwa watalii hao wametoka katika Nchi za Australia, Austria, Belgium, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, Poland, Urusi na Hispania huku wengine wakitokea Nchi za Switzerland, Uingereza na Marekani wakisafirishwa na Meli iitwayo “Le Bougainville”.

Watalii hao wameeleza kufurahishwa na upekee wa historia ya Magofu ya Kale, ustaarabu na utamaduni wa wakazi wanaoishi katika Hifadhi hiyo huku wakipongeza jitihada za dhati za kuboresha miundombinu ya utalii zilizofanywa na Serikali kupitia TAWA Hifadhini humo.

“Imekuwa ni safari nzuri kwetu kwasababu tumepata fursa ya kipekee kujifunza historia ya nchi hii nzuri ikiwa ni pamoja na kukutana na watu wa tamaduni mbalimbali kuona namna wanavyoimba na kucheza, nimependa sana hakika nimependa,” Dominick Alexandre mtalii kutoka Ufaransa

TAWA inaendelea kupokea wageni mbalimbali kutoka Kila Kona ya Dunia kupitia Hifadhi hiyo na Hifadhi nyingine zilizo chini ya usimamizi wake, ambapo katika kipindi cha Mwezi Februari kuanzia tarehe 03 mpaka tarehe 24 Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara imepokea Meli za watalii zipatazo sita zikiwa na jumla ya watalii 710 na bado inatarajia kupokea Meli nyingine za watalii ambao watatembelea Hifadhi hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here