Na Mwandishi wetu
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba, nchini Tanzania, Yordenis Despaigne Vera. Katika Mazungumzo wamejadiliana juu ya masuala mbalimbali yanayohusu namna ya kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Tanzania na Cuba na Chama Cha Mapinduzi na Chama Cha Kikomunisti cha Cuba (CPC).
Mazungumzo hayo yamefanyika leo Machi 5 2024 Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam, Balozi Vera ameishukuru Tanzania na CCM kwa jinsi ambavyo wamesimama na nchi hiyo katika nyakati zote.
Akizungumza Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Nchimbi amemhakikishia Balozi huyo kuwa CCM, chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kitafanya kila linalowezekana kuhakikisha urafiki na uhusiano kati ya Tanzania na Cuba kwa upande mmoja na CPC na CCM kwa upande mwingine unaenziwa na kuimarishwa zaidi kwa ajili ya manufaa ya pande zote mbili.
Amesema Kupitia majadiliano hayo, pamoja na masuala mengine, viongozi hao wa pande zote mbili, wamejadiliana na kuainisha maeneo yatakayofanyiwa kazi kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha ushirikiano kati ya Wananchi wa Tanzania na Cuba.
“Serikali za nchi zote mbili na vyama vinavyoongozwa na nchi hizo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza mipango ya kubadilishana utaalam katika maeneo mbalimbali na kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kiuchumi,”amesemaDk. Nchimbi.