Home KITAIFA Viongozi wamlilia Rais Hayati Mzee Mwinyi

Viongozi wamlilia Rais Hayati Mzee Mwinyi

Na Mwandishi wetu

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amewaongoza waombolezaji katika kutoa heshima za mwisho wakati wa kuaga mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Ali Hassan Mwinyi katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salam.

Akitoa salamu za pole Machi mosi kwa waombolezaji, Dk. Mpango uliohudhuliwa na viongozi mbalimbali amesema Hayati Mzee Mwinyi atakumbukwa kwa kuwa kisima cha hekima, chemichemi ya elimu na shule ya uzalendo uadilifu na uongozi.

Amesema Hayati Mwinyi alijitoa kwa dhati kulitumikia Taifa kwa moyo wake wote na kutoa mchango mkubwa kwa nafasi zote alizoshika katika utumishi wa umma.

“Hayati Ali Hassan Mwinyi amekuwa kielelezo cha kutetea na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, alikuwa na karama kubwa ya uongozi na alizingatia kwa dhati masharti ya uongozi ikiwemo uwajibikaji pamoja na kutoa mchango mkubwa katika kukuza matumizi ya lugha ya kiswahili na kuifanya kutambulika na kutumika kimataifa,”amesema Dk.Mpango.

Ameongeza kuwa Hayati Mwinyi aliasisi mageuzi ya kiuchumi na kisiasa hapa nchini, alijijengea sifa kubwa katika kuhamasisha kilimo bora pamoja na kuwa na bidii katika kumwabudu Mwenyezi Mungu.

Naye Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete amesema Mzee Mwinyi akiwa Rais alivunja baraza la mawaziri mara mbili wakiwa wote walikwenda kwenye baraza hakuonesha bashasha.

“Nawashukuru kwa miaka yote tumekuwa pamoja ila wenzangu naomba mwende mkajiuzulu alivyosema hivyo akaondoka tukawa tunajiuliza unakwenda je? Kuandika barua baada ya mda ikaja taarifa msiandike barua ikaja barua tuondoke ofisini twende nyumbani,”amesema Dk. Kikwete.

Ameeleza kuwa kwa mara ya pili haikuwa kama mwanzo waliona kwenye vyombo vya habari amevunja baraza la mawaziri alikuwa jasiri.

“Mzee Mwinyi alikuwa hajikwezi alikuwa mtu mwenye mapenzi na watu wote aliishi maisha ya kawaia ya uungwana na msikivu na alikuwa mtu wa kupokea maoni na zaidi ya yote alinifundisha kuwa na maamuzi hasa kwenye vitu vyenye maslahi na Taifa yeye ndiye baba wa mageuzi ya kiuchumi na siasa hapa nchini Tanzania,”ameeleza.

Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema leo ni majonzi kuondokewa na Mzee Mwinyi lakini siku ya furaha ya kusherekea maisha yake kwa mengi alifanya kutumikia Taifa hili kwani amekuwa na juhudi nyingi za kuleta maendeleo hasa kwenye nyanja ya uchumi na siasa.

Amesema Mzee Mwinyi alipokea nchi ikiwa kwenye matatizo makubwa lakini aliweza kupambana kuitoa nchi kwe uhaba wa uchumi.

“Mzee Mwinyi aliposhika uongozi hali ilivyokuwa wakati huo ilikuwa mbaya sana sasa hivi nchi tuna matatizo tuna upungufu wa sukari, matatizo ya umeme tuna matatizo ya maji lakini matatizo tuliyonayo sasa hivi ni madogo sana ukilinganisha na wakati wa Mwinyi aliposhika uongozi,”amesema Jaji warioba.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) , Abdulrhaman Kinana amesema sote leo ni mashahidi kwamba Hayati Mzee Mwinyi alifanya jitihada za kuitoa Tanzania kwenye chama kimoja kwenda kwenye mfumo wa vyama vyingi.

Amesema suala hilo halikuwa rahisi vilevile aliwapeleka kwenye uchumi hiari alifanya haya yote na mengine mengi kwa kumshirikisha Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere kwa lengo la kuhakikisha kwa mabadiliko yanafanyika kwa utulivu ili kulinda umoja wetu na amani yetu.

Tukio la kuagwa kwa Mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Ali Hassan Mwinyi katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam limehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia , Abiy Ahmed Ali, viongozi mbalimbali wa kitaifa, Mabalozi wa Mataifa mbalimbali, Viongozi wa Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini mbalimbali pamoja na Wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here